Friday , January 18 2019

Home / BIASHARA / WAKULIMA WA NDIMU BWEJUU WALILIA SOKO

WAKULIMA WA NDIMU BWEJUU WALILIA SOKO

Na mwandishi wetu, Zanzibar

Umoja wa Wakulima wa Ndimu wa Kikundi cha Juhudi Zetu kilichopo Bwejuu, mjini Unguja wametoa kilio chao cha kukosa soko la ndimu wanazozalisha kwa uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Wakizungumza na ugeni huo, wakulima hao wamesema kwa muda mrefu sasa wamekosa soko la uhakika la mazao yao kwa kukosa mnunuzi wa uhakika licha ya kulima kisasa na kupata mazao mengi.

Mmoja wa wakulima hao Bw. Shafi Hamadi Mussa amesema kuwa kwa muda mrefu sasa wamekosa soko la uhakika la mazao ya hali inayorudisha nyuma ari ya kuendelea kulima zao hilo.

“Tunakatishwa tamaa kwa kukosa soko la uhakika licha uwekezaji mkubwa tunaoufanya katika kulima kisasa,” Bw. Mussa alisema.

Bw. Mgana Khatibu Mgana, mkulima mwengine wa Umoja huo amesema changamoto ya ukosefu wa masoko inaweza kutatuliwa kwa kupatiwa mkopo nafuu wa kununulia mitambo ya uchakataji wa mazao ambayo itatumika kuongeza thamani kwa mazao yao.

“Tunauomba uongozi wa Benki ya Kilimo kutukopesha pesa za kununulia mitambo ya kuchakata mazao yetu ili kuepuka adha ya ukosefu wa masoko wa mazao haya,’ Bw. Mgana alisema.

Akijibu kilio cha wakulima hao, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga alisema Serikali imesikia kilio cha wakulima hao kwa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kusaidia kukabiliana na mapungufu ya wakulima nchini kote ili kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo na kuchagiza mapinduzi katika  kilimo nchini.

Aliongeza kuwa Benki yake imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa mazao yote ya wakulima nchini kwa kuanzia na baadhi ya mazao ili kupata picha halisi ya uhitaji wa rasilimali fedha kwa wakulima.

“Katika hatua za awali, Benki imeainisha Minyororo Kumi na Nne (14) ya Ongezeko la Thamani ya Bidhaa za Kilimo zitakayopewa kipaumbele katika kutoa mikopo ni pamoja na Kilimo cha Nafaka (Mahindi na Mchele), Kilimo cha Mazao ya Viwandani (Miwa na Korosho) na Ufugaji wa Ng’ombe (Ng’ombe wa Nyama na Maziwa),” Bw. Assenga alisema.

Aliongeza kuwa Benki inatoa mikopo kwa Kilimo cha Mbogamboga (Matunda, Mboga Mboga na Viungo), Kilimo cha Mbegu za Mafuta ya Kupikia (Alizeti na Ufuta) na kwa upande wa Kilimo cha Mazao ya Misitu ni Ufugaji wa Nyuki na mazao yake.

Mengine ni Kilimo cha Ufugaji wa Kuku (Kuku wa Kienyeji na wa Kisasa) na Kilimo cha Samaki (Ufugaji wa Samaki).

Bw. Assenga aliwaahidi wakulima hao kuwa TADB itafanyia kazi maombi yao ili kuona namna ya haraka itakayotatua changamoto zao.

Zaidi ya vipaumbele vilivyoainishwa, TADB pia imejipanga kusaidia minyororo mingine ya ongezeko la thamani ya mazao ya Kilimo kwa utaratibu   maalumu kadiri ya upatikanaji wa fedha ikiwa ni pamoja na kusimamia uendeshaji wa fedha mbalimbali zinazoelekezwa na Serikali ama wafadhili kwenye Sekta ya Kilimo. 

unnamed

Ugeni kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) wakikagua mashamba ya midimu wakati walipotembelea mashamba ya Umoja wa Wakulima wa Ndimu wa Kikundi cha Juhudi Zetu kilichopo Bwejuu, mjini Unguja.

A 1

Hali halisi ya kilimo cha ndimu kijijini Bwejuu, mjini Unguja.

A 2

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kulia) akioneshwa miundombinu ya umwagiliaji ya kilimo cha ndimu. Anayemuonesha ni Bw. Mgana Khatibu Mgana na (kushoto) na Bw. Kombo Haji Mussa (katikati).

A 3

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kulia) akiangalia namna midimu inavyomwagiliwa maji.

A 4

Meneja wa Mikopo wa TADB, Bw. Samuel Mshote (kushoto) akiangalia ndimu zilizoanguka kwa kukosa wateja. Kwa mujibu wa wakulima wa ndimu, ndimu huuzwa ikiwa katika hali ya kijani lakini changamoto za kukosa soko hupelekea ndimu za wakulima wa Kijiji cha Bwejuu kuivia mtini.

About Alex

Check Also

index

Mtoto wa Rais Trump atajwa kugombea nafasi ya urais wa Benki ya Dunia

Ivanka Trump binti wa rais wa Marekani, Donald Trump,ni moja ya majina yanayotajwa kuwania nafasi …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

twenty + fourteen =