Thursday , January 17 2019

Home / MCHANGANYIKO / Songwe Airport Yadhibiti ugonjwa wa Ebola

Songwe Airport Yadhibiti ugonjwa wa Ebola

unnamed

Afisa Afya Bw. Peter Alfred (katikati) akikagua hati ya kusafiria ya Bw. Paluku Ngahngondi (kushoto) Mkongo anayeishi Zambia, kabla ya kupanda ndege ya Fastjet kuja Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Afya Bi. Shukrani Nkonjeka akiwa kwenye mashine maalum inayompima kila abiria anayepita mbele yake kwa kupiga picha na kutoa mlio wa endapo anajoto kali la mwili.

1

Bi. Shukrani Nkonjeka, Afisa Afya akimpa maelezo kuhusiana na ugonjwa wa Ebola, mmoja wa wafanyakazi wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe (SIA), Bw. Fred Martin (kushoto).

2

Bi Shukrani Nkonjeka, Afisa Afya akiwapa maelezo yanayohusiana na ugonjwa hatari wa Ebola madereva wa taxi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Songwe (SIA).

3

Madereva wa taxi wa kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe (SIA), wakipokea vipeperushi vyenye maelezo mbalimbali yanayohusu ugonjwa hatari wa ebola kutoka kwa Afisa Afya, Bi. Shukrani Nkonjeka

………………………

MAAFISA Afya toka kitengo cha magonjwa ya dharura mkoa wa Songwe wameweka kambi  kwenye kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe (SIA), ili kubaini abiria wenye dalili za ugonjwa wa Ebola ulioibuka hivi karibuni kwenye nchi ya jirani ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Kiwanja cha Kimataifa cha Songwe kilichojengwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) mwaka 2012 kinapokea abiria 500,000 kwa mwaka kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwemo nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. TAA inahudumia viwanja 58 vilivyopo chini ya serikali.

Afisa Afya Bw. Peter Alfred amesema wamefunga mashine maalum na ya kisasa kiwanjani hapo, ambayo abiria akipita umbali wa mita tano hadi 10 inampiga picha na kuonesha joto alilonalo mwilini, na endapo atakuwa na joto la nyuzijoto 37.5 mashine hiyo itatoa mlio wa kengele.

Bw. Alfred amesema abiria atakayekuwa na joto hilo, atachukuliwa na kupelekwa eneo maalum lililotengwa umbali wa mita 300 kutoka eneo la kiwanja cha ndege na baadaye kupelekwa hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa ajili ya matibabu zaidi.

Hata hivyo, amesema mbali na kuangaliwa kwa abiria wenye joto kali la mwili, pia hukagua na kupata maelezo binafsi kwa kujaza fomu maalum kwa abiria wote wanaopita kwenye kiwanja hicho wakitokea kwenye nchi za Kongo, Guinea, Sierra Leone, Mali, Nigeria, Liberia, Senegal, Marekani na Hispania kutokana na nchi hizo ziliwahi kukumbwa na ugonjwa huo. 

“Hadi  sasa tangu zoezi hili limeanza baada ya kupatikana kwa taarifa za ugonjwa kuwa hapo Kongo, bado hatujapata mgonjwa mwenye dalili hizo na tunaendelea kuudhibiti kwani hapa ni njia kuu kwa abiria wanaotoka Kongo ni wengi,” amesema Bw. Alfred.

Bw. Alfred amesema ugonjwa wa Ebola unasababishwa na virusi vya Ebola vinavyoingia mwilini mwa binadamu na wanyama kupitia puani, masikioni na machoni, na huambukiza kwa kugusa majimaji ya mwili toka kwa mtu aliyeambukiwa virusi hivyo, yakiwemo matapishi, damu, jasho, mkojo, machozi, kamasi na mate.

Pia binadamu anaweza kupata ugonjwa huu kwa kugusa au kuosha maiti ya aliyefariki kwa ugonjwa huu au kugusa shuka, godoro, nguo na blanketi lililotumika na mgonjwa; pia kuchomwa na sindano au vifaa visivyo safi na salama vilivyotumiwa na mgonjwa wa ebola; au kula matunda yaliyoliwa nusu na wanyama na kugusa mizoga au kula wanyama pori kama nyani, sokwe na popo.

Bw. Alfred amesema dalili za ugonjwa huu zinaanza kujitokeza kati ya siku mbili hadi 21 baada ya kupata maambukizi, ambapo mgonjwa hupata homa kali ya ghafla, maumivu ya kichwa, maumivu ya mwili, misuli na viungo, vipele mwilini, kuvia damu chini ya ngozi, kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni, machoni, kuharisha na kutapika kunakoweza kuambatana na damu.

Hata hivyo, Bw. Alfred amesema ugonjwa huu hauna tiba maalum wala chanjo, lakini mgonjwa hupatiwa tiba saidizi kulingana na dalili alizonazo kama vile kushusha homa na maumivu, kuongezewa damu na maji mwilini na tiba lishe.

Bw. Alfred amesema wananchi wanaweza kujikinga na ebola kwa kuepuka kusalimiana kwa kupeana mikono au kukumbatiana, kuepuka kugusa majimaji yaliyotoka mwilini mwa mgonjwa au kuosha maiti, kuacha kutumia godoro, shuka na nguo za mgonjwa na pia wawahi haraka kituo cha kutolea huduma za afya endapo wataona dalili za ugonjwa wa ebola.

 

IMETOLEWA NA KITENGO CHA SHERIA NA MAHUSIANO, MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA.

 

About Alex

Check Also

HA2

WAKULIMA KUSAJILIWA NA KUPATIWA VITAMBULISHO NCHINI

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akifungua  mkutano wa kitaifa wa wadau wa Tumbaku nchini leo …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

3 + seven =