Monday , February 18 2019

Home / MICHEZO / “NITAIMARISHA SOKA LA VIJANA NCHINI” MULAMU

“NITAIMARISHA SOKA LA VIJANA NCHINI” MULAMU

mulamu!

Na Thobias Robert-Maelezo

Kampeni za  uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zimefunguliwa rasmi na Kamati ya Uchaguzi inayoongozwa na mwenyekiti wake Revocatus Kuuli huku wagombea wake wakianza kumwaga sera zao kwa wajumbe ambao  ndiyo wapiga kura wao.

Mmoja wa wagombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Shirikisho  hilo, Mulamu Nghambi  ameahidi kuendeleza na kuimarisha soka la vijana ili kuzalisha wachezaji bora kwa ajili ya timu ya Taifa, (Taifa Stars).

Mulamu ameyasema leo wakati akizungumza na Waaandishi wa Habari katika ufunguzi wa kampeni yake ya kusaka kura ili aweze kupata nafasi hiyo huku akinadi sera za mipango ya muda mfupi na muda mrefu ambayo ataitekeleza kama  ridhaa ya wapiga kura katika nafasi hiyo.

“Tutahakikisha kila mkoa unaendesha programu ya kuendeleza vijana wenye umri wa miaka 13 (U-13) kupitia shule za msingi na sekondari kwa kushirikiana na TAMISEMI. Shirikisho litahakisha kila klabu inakuwa na timu za vijana ambazo zitakuwa na walimu na ambao watafuata  programu zinazoeleweka,” alifafanua Mulamu.

Aliongeza kusema kuwa, mfumo huo ukifanikiwa  watashirikiana na vilabu vya mpira wa miguu nchini, ambapo  utasaidia kutengeneza timu bora za taifa ambazo zitashiriki katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na  kimataifa.

“Hakuna  taifa lolote linaloendelea kisoka bila kuwekeza katika soka la vijana, ambapo soka hili linatakiwa kuanzia ngazi ya chini ili vijana hawa wakue katika mazingira ya soka na siyo kuanza kutayarishwa wakiwa wakubwa” aliongeza Mulamu.

 Mbali na kuimarisha soka la vijana, mgombea huyu  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA), ameahidi kuimarisha  na kusimamia udhibiti na uwazi wa mapato na matumizi ya fedha za Shirikisho kwa kuziba mianya ya rushwa na kuzuia  matumizi ya fedha yasiyo rasmi

“Nitapambana kuongeza mapato kwa kutumia njia ya kisasa ya mawasiliano yaani digital platforms kwa kufanya miamala kwa kutumia simu za mkononi kupitia maunzi laini (Application) yetu ambayo tutaitengeneza,” Mulamu alisisitiza jambo hilo.

Endapo atachaguliwa, Mulamu  ameahidi kushirikiana na viongozi wengine watakaopewa ridhaa na wapiga kura kuongeza idadi ya vilabu shiriki katika Ligi Kuu Tanzania  Bara kutoka vilabu 16 hadi 20 ili kuongeza  ufanisi wa soka nchini na kupeleka ligi hiyo mikoani.

Wagombea wengine katika nafasi hiyo ni pamoja na Michael Wambura, Mtemi Ramadhani, Stephen Mwakibolwa na Robert Selasela. Awali aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo ni Wallace Karia ambaye anagombea nafasi ya urais wa shirikisho hilo.

Uchaguzi huu utafanyika Agosti 12, mwaka huu, kufuatia kumalizika kwa muda wa uongozi uliopo madarakani kwa mujibu wa katiba ya shirikisho hilo.TFF ilikuwa iliongozwa  na Jamali Malinzi  kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2013.

About Alex

Check Also

9832670-6706055-image-a-15_1550177026096

CHELSEA YAPETA UGENINI EUROPA LEAGUE,YAICHAPA 2-1 MALMO

Ross Barkley na Olivier Giroud wakipongezana baada ya wote kuifungia Chelsea katika ushindi wa ugenini …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

17 + 15 =