Wednesday , April 24 2019

Home / MCHANGANYIKO / KAMATI YA MIUNDOMBINU YARIDHISHWA NA UJENZI UWANJA WA NDEGE WA MWANZA

KAMATI YA MIUNDOMBINU YARIDHISHWA NA UJENZI UWANJA WA NDEGE WA MWANZA

1

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA) Bw, Richard Mayongela akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu hawapo pichani wakati walipokagua uwanja wa ndege wa Mwanza,  kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi) Mhe. Elias John Kwandikwa na kulia ni Meneja wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS mkoa wa Mwanza Eng. Marwa Rubirya na Meneja uwanja wa ndege wa Mwanza Bi, Esther Madale.

2

Muonekano wa barabara ya kutua na kurukia ndege ambayo ujenzi wake unaendelea katika uwanja wa ndege wa Mwanza, uwanja huo unaboreshwa ili uwe na hadhi ya kimataifa.

3

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi) Mhe. Elias John Kwandikwa akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu walipokagua ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza.

4

Muonekano wa Kivuko cha MV Misungwi II ambacho kinajengwa na kampuni ya Songoro Marine mjini mwanza kikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake, kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba abiria elfu moja na magari 36 kwa wakati mmoja  kinatarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka huu.

5

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mh. John Mongela akiwa pamoja na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakipata maelezo ya mradi wa ujenzi wa kivuko cha MV Misungwi II toka kwa Bw, Mohamed Salum mwakilishi wa mkandarasi  Songoro Marine anayejenga kivuko hicho mjini Mwanza.

3

Mhandisi mkazi wa uwanja wa ndege wa Mwanza  Geofrey Asulumenye akifafanua jambo kwa wajumbe wa kamati ya bunge ya Miundombinu walipokagua ujenzi wa uwanja wa ndege huo.

…………………..

Kamati ya Bunge ya Miundombinu imeeleza kuridhishwa kwake na ujenzi wa Barabara, Kivuko na uwanja wa ndege mkoani Mwanza na kusisitiza hali hiyo ikiendelea itawezesha Serikali kupata huduma zinazowiana na thamani ya fedha.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Moshi Sulemani Kakoso amesema kamati yake imeridhika kwa hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa barabara ya Usagara-Kisesa KM 16.9, ujenzi wa MV misungwi II na upanuzi na ukarabati wa uwanja wa ndege wa Mwanza.

“Hakikisheni jengo la abiria lenye hadhi ya kimataifa linajengwa haraka katika uwanja wa ndege wa Mwanza  ili kuwiana na urefu wa uwanja huu na hivyo kuvutia ndege nyingi katika ukanda wa Afrika Mashariki kutua Mwanza”, amesema Mhe. Kakoso.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Hawa Mchafu ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), kuharakisha ujenzi wa uzio katika uwanja  wa Mwanza ili kurahisisha huduma za usafi, utunzaji wa mazingira na usalama wakati wote.

Nae mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Suzan Kiwanga amewataka wasimamizi wa miradi ya ujenzi nchini  kuhakikisha wanatoa fursa za ajira kwa wanawake pale inapoonekana wana sifa za kufanya kazi husika ili kukuza uchumi wa jamii na kuhamasisha wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi na uhandisi.

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anaeshughulikia (sekta ya ujenzi), Mhe. Elias John Kwandikwa amesema Serikali itaendelea kuhakikisha barabara na viwanja vya ndege vinajengwa kwa muda mfupi ili kuokoa gharama na pale itakapohitajika kulipa fidia kwa wananchi Serikali haitamuonea mtu.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea na sera ya kuwawezesha wakandarasi wazalendo ili kuwajengea uwezo katika ujenzi wa miradi ya kati na mikubwa ili kukuza uchumi wa nchi.

Kamati ya Bunge ya Miundombinu iko katika ziara ya kutembelea miundombinu inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, na Mara.

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano

About Alex

Check Also

4-4

SERIKALI YAWAJAZA MAPESA BILIONI 688 WAKANDARASI WA MRADI WA UMEME WA RUFIJI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James akimkabidhi Katibu Mkuu wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

three × 2 =