Thursday , February 21 2019

Home / MCHANGANYIKO / WANAWAKE KUPEWA KIPAUMBELE MIRADI YA UJENZI

WANAWAKE KUPEWA KIPAUMBELE MIRADI YA UJENZI

????????????????????????????????????

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro Mhandisi Moses Kiula, akizungumza na waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake (hawapo pichani), kutoka mikoa yote ya Tanzania bara, mkoani Morogoro, wakati wa ufunguzi wa semina elekezi  kwa ajili ya kuwajengea ujuzi, uwezo na njia mbadala za kuongeza idadi ya wanawake katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara.

????????????????????????????????????

Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wanawake katika kazi za barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Rehema Myeya,  akifafanua jambo kwa waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake (hawapo pichani), mkoani Morogoro, wakati wa ufunguzi wa semina elekezi kuhusu njia mbadala za kuwahamasisha wanawake kushiriki kwa wingi katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara.

3

Baadhi ya waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake kutoka mikoa yote ya Tanzania bara wakisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni rasmi ambaye ni Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro Mhandisi Moses Kiula, wakati wa ufunguzi wa semina elekezi iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ujenzi cha Morogoro, mkoani humo.

????????????????????????????????????

Mratibu wa masuala ya jinsia kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Bi. Diana Kahigwa akizungumza na waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake (hawapo pichani), kutoka mikoa yote ya Tanzania bara, wakati wa ufunguzi wa semina elekezi kuhusu namna  ambavyo Serikali inavyoshughulikia masuala hayo hasa katika ushiriki wa wanawake katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara, mkoani Morogoro.

????????????????????????????????????

Mratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake kutoka mkoa wa Shinyanga Mhandisi Jessica Manang, akichangia mada katika semina elekezi iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ujenzi cha Morogoro. Semina hiyo imehudhuriwa na waratibu wa mikoa yote Tanzania bara kutoka ofisi za mameneja wa  mikoa wa Wakala wa Barabara (TANROADS).

????????????????????????????????????

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro Mhandisi Moses Kiula, akiwa katika picha ya pamoja na waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake kutoka mikoa yote Tanzania bara katika semina elekezi iliyofanyika mkoani Morogoro katika Chuo cha Ujenzi cha Morogoro.

……………..

Uwiano wa wanawake katika miradi mingi ya ujenzi nchini ikiwemo matengenezo na usimamizi wa barabara unaelezwa kufikia asilimia 6 na 7 kati ya wahandisi 100 ukilinganisha na wanaume katika Sekta ya hiyo.

Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara(TANROADS), mkoa wa Morogoro Mhandisi Moses Kiula, wakati akifungua semina elekezi kwa waratibu wa shughuli za ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara nchini na kufafanua kuwa hali hiyo inatokana na ushirikishwaji mdogo wa wanawake katika kazi hizo.

 Aidha, Mhandisi Kiula,  amesisitiza umuhimu wa semina hiyo kwa waratibu hao ili kuwajengea uwezo, ujuzi na njia mbadala za kuongeza idadi ya wanawake watakaoshiriki katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara na pia  kuhamasisha wanawake wengine zaidi kushiriki kazi hizo.

“Serikali sasa inalenga kuwawezesha makadarasi wanawake kufikia madaraja ya juu ya ukandarasi ili kuweza kuinua kipato chao na kuondokana na umasikini katika familia na jamii kwa ujumla”, amesisitiza Mhandisi Kiula.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo elekezi yatawasaidia katika kupambanua masuala muhimu yatakayoweza kurahisisha uratibu na usimamizi mzuri katika utendaji wa kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara kwa ufanisi zaidi.

“Ni maratajio yangu mkimaliza mafunzo haya mtatekeleza kazi zenu kwa ufanisi zaidi na kuleta matokeo chanya  kwa jamii na Taifa”, amesema Mhandisi Kiula

Kwa upande wake Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wanawake katika kazi za barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Rehema Myeya, amesema kuwa kazi kuu za waratibu hao ni kuwahamasisha wanawake kushiriki kwa wingi katika kazi za barabara katika mikoa yote ili kutanua wigo wa maendeleo katika jamii na mafanikio katika kazi hizo.

Mhandisi Myeya, ametaja mada zitakazojadiliwa katika semina hiyo kuwa ni masuala ya jinsia na namna ambavyo Serikali inayashughulikia ikiwemo sheria ya ujenzi na namna inavyosisitiza ushiriki wa wanawake na kuipitia sheria ya manunuzi na kuona maeneo ambayo yanatoa kipaumbele kwa wanawake.

Mada nyingine ni kuangalia mchakato wa usajili kwa makampuni ya wanawake, kupitia mwongozo wa kuimarisha ushiriki wa wanawake katika kazi za barabara na masuala mtambuka, namna ya kuandaa zabuni ambazo zinaakisi mahitaji ya wanawake na ufanisi wa teknolojia ya nguvu kazi katika kufanya matengenezo ya barabara.

Ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara kitaifa ulianza mwaka 1992 katika mikoa ya Mbeya, Tanga, Shinyanga, Mwanza na Mtwara na hii ni kutokana na kazi hizo kufanywa na wanaume hasa kwenye nyanja za makandarasi na wahandisi washauri.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

About Alex

Check Also

3

HALMASHAURI YA WILAYA YA KISARAWE YAPITISHA BAJETI YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 30

Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Hamisi Dikupatile akizungumza na wajumbe wa kikao cha …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

4 − 2 =