Friday , March 22 2019

Home / MCHANGANYIKO / DC REGINA CHONJO:HAKUNA HAKI BILA YA WAJIBU

DC REGINA CHONJO:HAKUNA HAKI BILA YA WAJIBU

BN640246

Na. Andrew Chimesela – Morogoro

Baraza la wafanyakazi la Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro limetakiwa kuwa chachu ya wafanyakazi wa Mkoa huo na kuwakumbusha wafanyakazi hao kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili waweze kupewa haki na stahiki zao bila kikwazo pindi wanapolazimika kuzidai haki hizo.

Kauli hiyo imetolewa Aprili, 15 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Regina Chonjo wakati wa kikao cha uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi la Mkoa huo kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambapo pia ulifanyika uchaguzi wa Viongozi wa Baraza hilo.

Mhe. Chonjo amesema, watumishi wa Serikali wanazo changamoto mbalimbali katika utumishi wao ikiwemo nyongeza ya mishahara, posho, madeni, mafunzo, kupanda vyeo na changamoto nyingine, zote hizi ni haki zao za msingi ambazo zitatekelezwa iwapo kuna uwajibikaji kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu, kwa kuwa hakuna haki bila uwajibikaji.

“Katika utumishi wetu kuna kitu kinaitwa haki na wajibu, na ili uweze kupata haki ni lazima utekeleze wajibu wako. Lakini vile vile wajibu unaweza usitekelezeke kama yule anayetakiwa afanye wajibu fulani haki yake haioni mbele kama ipo”. Alisema Mhe. Chonjo.”

Aidha, Mhe. Chonjo amewataka viongozi na wajumbe wa Baraza hilo kuwa chachu kwa wenzao huku wakijua kuwa kazi yao kubwa ni kuwakumbusha wanaowawakilisha kuwajibika ipasavyo wawapo kazini na kuwa na nidhamu ya kazi huku wakijua kuwa Baraza hilo ni muhimili wa wajibu na haki kwa wafanyakazi wa Mkoa wao.

Naye Katibu wa TUGHE Mkoa wa Morogoro Bi. Sara Rwezaula amesikitishwa na Baraza hilo la wafanyakazi kwa kutofanya vikao vyake ambavyo ni vya kisheria tangu mwaka 2016 na kuwataka Viongozi ngazi ya Mkoa na wa Baraza kubadilika ili baraza hilo liwe na maana kwa Wafanyakazi na kuwaletea tija.

Aidha, Bi. Rwezaula ameuomba uongozi wa Mkoa wa Morogoro kulithamini Baraza hilo ikiwa ni pamoja na kufanyika vikao, ulipaji wa posho kwa wajumbe wake na kutoa mapema taarifa ya vikao vinavyotakiwa kufanyika hususan kikao cha kupitisha Bajeti ya Mkoa ili wajumbe wake wapate muda wa kuchangia mawazo yao kwa lengo la kuiboresha bajeti hiyo.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw. Lucas Mwaisaka amekiri kuwa vikao vya Baraza hilo havijafanyika kwa muda mrefu kwa sababu mbalimbali hata hivyo  ameahidi kuwa vikao vya Baraza hilo kuanzia sasa vitatekelezwa kikamilifu na kwa mujibu wa sheria ya vikao hivyo.

Kabla ya Mgeni rasmi kuzindua Baraza hilo, ulifanyika uchaguzi wa Katibu na Katibu Msaidizi wa Baraza hilo kwa kuwa kimuundo Mwenyekiti  wa Baraza ni Katibu Tawala wa Mkoa. Katika uchaguzi huo Bi. Angela Mono amechaguliwa kuwa Katibu na Bw. Emannuel Mazengo amekuwa Katibu Msaidizi. Wachaguliwa wote ni watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Mkoa lina majukumu mengi mojawapo ni kushauri Mpango wa Bajeti ya Mkoa, na linaundwa na Katibu Tawala wa Mkoa ambaye ndiye Mwenyekiti, Wakuu wote wa Idara na Vitengo, Makatibu Tawala wa Wilaya, wajumbe wa kuchaguliwa na wajumbe kutoka TUGHE Taifa, Mkoa na Wilaya.

 

About Alex

Check Also

IMG_7568

Lishe Endelevu kumaliza Tatizo la Udumavu Mkoa wa Rukwa

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule akitoa nasaha wakati wa kufungua kikao cha …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

20 + thirteen =