Thursday , March 21 2019

Home / MCHANGANYIKO / MPINA AWATAKA WAWEKEZAJI WA VIWANDA VYA PUNDA KUONGEZA BEI

MPINA AWATAKA WAWEKEZAJI WA VIWANDA VYA PUNDA KUONGEZA BEI


Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina(mwenye miwani) akikagua kiwanda cha
kuchinja Punda cha Hua Cheng Limited kilichopo nje kidogo ya mji wa
Dodoma alichokifungua hivi karibuni leo. (Picha na Jumanne Mnyau)

Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina(mwenye miwani) akipokea maelezo ya
usindikaji wa nyama Punda kutoka kwa mfanyakazi wa wa kiwanda cha
kuchinja Punda cha Hua Cheng Limited Elizabeth Peter.(Picha na Jumanne
Mnyau)

Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Luhaga Mpina(mwenye miwani)
akitembezwa katika kiwanda cha
kuchinja  Punda  cha Hua Cheng Limited kilichopo nje kidogo ya
mji wa Dodoma  alichokifungua  hivi karibuni na Meneja Mkuu wa kiwanda hicho
bwana Xun Long Go .(Picha na Jumanne Mnyau)

Na John Mapepele, Dodoma

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina
amewataka wawekezaji wa viwanda vya kuchinja Punda nchini kupandisha
bei ya kununua wanyama hao badala ya shilingi laki mbili ya sasa kwa
punda mmoja ili kudhibiti utoroshaji wa mifugo nje ya nchi ambapo
inakadiriwa kuwa zaidi ya mifugo elfu kumi inatoroshwa mipakani kwa
siku kwenda nje ya nchi inakonunuliwa kwa bei ya juu.

Akizungumza
leo baada ya kufanya ziara ya kushitukiza katika Kiwanda cha Punda
cha Hua Cheng Limited kilichopo nje kidogo ya mji wa Dodoma
alichokifungua hivi karibuni, Waziri Mpina alisema bei hiyo haiendani
na gharama halisi ya ufugaji wa Punda hali inayowafanya wafugaji
kuwatorosha mifugo na kulikosesha taifa mapato makubwa.

Alisema
ili punda aweze kufikia hatua ya kuchinjwa inachukua kiasi cha miaka
miwili ambapo gharama zake za ufugaji zinakuwa juu ukilinganisha na
bei ya shilingi laki mbili anayouzwa kwa wenye viwanda vya punda
nchini.

Aidha alisema kumekuwa na utoroshaji mkubwa wa mifugo wanaokadiriwa
kufikia takribani 1,614,035 kwa mwaka unaofanyika kwenye mipaka ya
nchi yetu ambapo takribani shilingi bilioni 32.28 zinapotea kama ushuru
na takribani shilingi bilioni 24.21 zinapotea kutokana na kodi ya
mapato ambayo ingelipwa kwa nyama ambayo ingeuzwa hapo nchini.

Aidha
Mpina ameunda tume ya wataalam kutoka Wizarani kwa ajili ya kuja
kufanya tathmini kama kiwanda hicho kimetimiza masharti yote
yaliyotolewa na Serikali baada ya kukifungua Februari mosi mwaka huu
ambapo alisema ikibainika kuwa kiwanda hakijakidhi masharti
yaliyotolewa na Serikali kitachukuliwa hatua kali zaidi za kisheria
ikiwa ni pamoja na kukifungia kufanya kazi zake.

Aliyataja
baadhi ya masharti yaliyotolewa na Serikali wakati wa kukifunga kiwanda
hicho Julai 2017 kuwa ni pamoja na kuwa na ranchi za punda, kuboresha
kosaafu za Punda nchini, kuunda na kuingia mikataba na vikundi vya
wafugaji wa Punda na kuwa na Punda wasiopungua mia tatu katika eneo la
kuhifadhia mifugo kabla ya kuchinjwa ili kuwa kuhakikisha kwamba
mifugo wanaangaliwa kwa wiki mbili kabla ya kuchinjwa ili wawe
katika ubora wa kimataifa.

Waziri Mpina alisema uwekezaji wa
aina hiyo wa kuongeza thamani ya mazao ya mifugo ni moja ya vipaumbele
vya wizara yake kwa sasa ili kuchochea kwa kasi kufanikisha azma ya
Tanzania ya viwanda.

Aidha aliwahakikishia wawekezaji wa
kiwanda hicho kuwa endapo watakuwa wamekamilisha masharti atawapa kibali
cha kudumu ambapo pia atawaongezea idadi ya kuchinja Punda kutoka
punda 20 wa sasa ili vijana wengi wapate ajira na kiwanda kiweze
kuchangia zaidi katika mapato ya Serikali.

Mpina aliwahimiza
wawekezaji hao kuhakikisha wanawasaidia wafugaji katika kuongeza
uzalishaji, kupambana na maradhi, upatikanaji wa maji na malisho kwa
mifugo.

Alisema idadi ya punda waliopo nchini ni 520,000 tu hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kuongeza uzalishaji.

Naye
Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Xun Long Go alimshukuru Waziri Mpina
kwa kufungua kiwanda hicho ambapo amesema hadi sasa kiwanda
kimezalisha na kuuza tani 224 za nyama ya Punda kwenda nchini China
na Vietinam ambapo pia tani 52 za ngozi ya Punda ilizalishwa na kuuzwa
kuanzi mwezi Februari, 2018.

Alisema kiwanda hicho kimeajiri watanzania 55 ambapo hadi sasa kina punda 88 katika maeneo ya Chalinze na Zuzu mkoani Dodoma.

Kaimu
Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko wa Wizara ya Mifugo na
Uvuvi, Lucia Chacha aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kwa kubuni
mbinu za kuwasaidia wafugaji kwa kuwapatia elimu bora zaidi ya ufufaji
wa punda ili waweze kuwazalisha kwa wingi zaidi kuliko ilivyo sasa

Hivi
sasa Tanzania ina viwanda viwili tu vya kuchinja na kuuza nyama ya
punda ambavyo ni kiwanda cha Punda cha Huacheng Limited kilichopo nje
kidogo ya mji wa Dodoma na Kiwanda cha Fang Hua kilichopo Shinyanga
ambavyo vyote vimepewa kibali cha kuchinja Punda 20 kwa siku kila
kimoja.

About Alex

Check Also

IMG_7568

Lishe Endelevu kumaliza Tatizo la Udumavu Mkoa wa Rukwa

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule akitoa nasaha wakati wa kufungua kikao cha …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

thirteen − 3 =