Wednesday , January 16 2019

Home / BIASHARA / BENKI KUU YA TANZANIA YAIDHINISHA KUUNGANISHA BENKI ZA TWIGA NA TPB

BENKI KUU YA TANZANIA YAIDHINISHA KUUNGANISHA BENKI ZA TWIGA NA TPB

IMG_3294

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Bernard Kibesse, akizungumza na waandishi wa habari wakati Benki Kuu ilipotangaza kuidhinisha kuunganisha benki za Twiga Bancorp Ltd na TPB bank Plc Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

IMG_3230

Kulia, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Bernard Kibesse akiteta jambo na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mabenki wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Kened Nyoni, kabla wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari leo asubuhi Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

IMG_3337

Waandishi wa habari katika mkutano wao na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Bernard Kibesse leo asubuhi. Katika mkutano huo, Benki Kuu ya Tanzania ilitangaza uamuzi wake wa kuidhinisha kuunganishwa kwa benki za Twiga Bancorp na TPB Bank Plc.

………………….

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeidhinisha ombi la kuunganisha benki ya Twiga (Twiga Bancorp Ltd) na benki ya TPB (TPB Bank Plc) na kuwa benki moja kuanzia kesho tarehe 17 Mei 2018.

Benki hiyo itaitwa TPB Bank Plc, ametangaza Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Bernard Kibesse, Jumatano tarehe 16 Mei 2018 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

BoT, ambayo ina mamlaka ya kusimamia mabenki na taasisi za fedha kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, ilichukua usimamizi wa Twiga Bancorp kutokana na benki hiyo kuwa na upungufu mkubwa wa mtaji.

Uamuzi huo wa kuziunganisha benki hizo ambazo zote zinamilikiwa kwa sehemu kubwa na Serikali ya Tanzania unahitimisha jukumu la BoT kusimamia uendeshaji wa benki ya Twiga tangu tarehe 28 Oktoba 2016.

“Muungano huu utaifanya Benki Kuu kusitisha usimamizi wa benki ya Twiga na mambo yote kuhusiana na benki hiyo yatafanywa na benki ya TPB kuanzia tarehe 17 Mei 2018,” alisema Naibu Gavana Dkt Kibesse katika taarifa yake kwa waandishi wa habari.

Alieleza kwamba Benki mpya ya TPB itakuwa na mtaji wa kutosha kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006. Aidha, uamuzi huo unamaanisha kwamba wateja, wafanyakazi, mali na madeni yote ya benki ya Twiga yatahamishiwa TPB Bank Plc.

Dkt. Kibesse alisema uamuzi wa kuidhinisha kuziunganisha benki hizo umechukuliwa ili kuboresha uangalizi na utendaji wa benki zinazomilikiwa na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. “Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha,” alisema Dkt. Kibesse.

 

About Alex

Check Also

PICHA 1

TRA YAKUSANYA TRILIONI 7.9 KATIKA KIPINDI CHA MIEZI 6 YA MWAKA WA FEDHA 2018/19

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Richard …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

14 − ten =