Thursday , February 21 2019

Home / MCHANGANYIKO / HAMZA TEMBA NURU ILIYOPOTEA GHAFLA IKIHITAJIKA KATIKA TASNIA YA MAWASILIANO

HAMZA TEMBA NURU ILIYOPOTEA GHAFLA IKIHITAJIKA KATIKA TASNIA YA MAWASILIANO

 

Na Munir Shemweta

‘’Pamoja kaka’’, hiyo ni kauli aliyokuwa akipenda kuitamka Hamza Temba mara tu anapokubaliana na ushauri wangu.

Temba afisa habari Wizara ya Maliasili na Utalii ni kijana mtanashati aliyependa kujifunza mambo kwa lengo la kutaka kuboresha utendaji wake wa kazi katika tasnia ya mawasiliano.

Namuita kijana anayependa kujifunza kutokana na tabia yake ya kuomba ushauri mara kwa mara pale anapoona kuna jambo linamtatiza katika kazi zake.  Naweza kusema kuwa mimi nilikuwa mmoja wa washauri wake wakuu katika masuala mabalimbali na hilo limemenifanya kuwa karibu sana naye.

Kufuatia ari ya kutaka kujifunza na kujua mambo mapya haikushangaza wanafunzi wa chuo  cha waislamu Morogoro (MUM)  kuona Temba akiwa karibu sana wanafunzi waliomtamgulia darasa kiasi cha baadhi yao kudhani alikuwa akisoma na wanafunzi  wa shahada ya Mawasiliano ya Umma waliomaliza mwaka 2008.

Ukaribu wangu na Temba ulianzia Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM) hasa baada ya kubaini kuwa mimi nilipitia ‘news room’ hivyo lengo lake lilikuwa kutaka kuchota utaalamu ili atakapoanza kufanya kazi  iwe rahisi kwake kufanya kazi kwa uafanisi.

Alipofaulu usaili kwa ajili ya kupata ajira, Temba alinifuata ofisini Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na kunipa taarifa ya yeye kufaulu usaili wa afisa habari na kutakiwa kuripoti kituo cha kazi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Lengo la kuja kwangu ni kutaka ushauri kuhusu suala la kuenda mkoani Rukwa kwani hakufurahishwa kupangiwa mkoani humo.

Mimi nilimshauri sana aende huko ili aweze kupata changamoto na kumsisitizia kuwa mkoa wa Rukwa hauna shida yoyote na anaweza kufanya kazi asiangalie historia kuwa mkoa wa Rukwa hauna mazingira rafiki ya kufanya kazi.

Baada ya kutafakari sana, Temba alikubaliana na ushauri wangu lakini kwa masharti la kutaka kuangalia mazingira kwanza na ikishindikana aaangalie masuala mengine ikiwa ni pamoja na kijishughulisha na biashara, lakini mimi niliendelea kumpa moyo kuwa anaweza kufanya kazi katika mkoa huo bila shida yoyote.

Temba alienda mkoa wa Rukwa kwa ajili ya kuanza kazi na alipofika huko alinieleza kwa njia ya simu kuwa alisharipoti kituo chake cha kazi na kutambulishwa kwa uongozi akiwemo mkuu wa mkoa wa Rukwa wakati huo Daniel Ole Njolay.  Tofauti na alivyofikiri katika kipindi kifupi Temba alianza kupenda kazi na kilichompa faraja zaidi ni ushirikiano alioupata kwa uongozi wa mkoa hasa mkuu wa mkoa Balozi Njolay. Utendaji kazi wa Temba uliimarika zaidi pale alipoanzisha Blog ya mkoa wa Rukwa ambayo kwa kiasi kikubwa iliutangaza mkoa pamoja na shughuli zake.

Wakati Temba akiwa katika ‘’Peak’’ kama wanavyosema vijana wa mjini yalitokea mabadiliko katika mko wa Rukwa aliyekuwa mkuu wa mkoa huo Njolay aliteuliwa balozi wa Tanzania nchini Nigeria na Injinia Stela Manyanya kuchukua nafasi yake, Temba alinipigia simu na kunieleza mabadiliko hayo huku akiwa na wasiwasi wa kupata ushirikiano kama alioupata kwa Njolay.

Nilimtoa shaka na kumpa moyo kutokana na kazi kubwa aliyoifanya katika kuuhabarisha umma na kumueleza kuwa nina imani Manyanya atashirikiana naye vizuri. Hata hivyo, ilikuwa vigumu Temba kuniamini lakini alinijibu kwa kunieleza kuwa ngoja tuone. Baada ya muda Temba aliniambia kuwa yale niliyomuekeza alianza kuamini kwani anafanya kazi kwa karibu sana na Injinia Manyaya kuliko hata ilivyokuwa kwa Njolay. Kwa mujibu wa marehemu Temba, mhe Manyanya alimtumia hata katika ‘’kudesign’’ kipeperushi kwa ajili ya harakati zake za kutaka kuwania ubunge jimbo la Nyasa mkoa wa Ruvuma

Siku moja Temba akiwa Dar es Salaam kikazi alinieleza nia yake kutaka kubadilisha mazingira ya kazi akiwa na maana kutoka Sekretarieti ya Mkoa na kuuingia Serikali Kuu, nilimueleza kuwa hilo ni jambo jema litakalosaidia kupanua wigo wake katika tasnia ya habari. Temba alipendelea zaidi kufanya kazi Wizara Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Jitihada zake za kuhamia wizara hiyo ziligonga mwamba na alibahatika kuenda Wizara ya Maliasili na Utalii.

Alipoanza kazi wizara hiyo, alionesha kufurahishwa na mazingira ukilinganisha na sekretarieti ya mkoa wa Rukwa ingawa kulikuwa na changamoto kadhaa. Nilimshauri kikubwa katika wizara hiyo ni kufanya kazi kwa kwa kujituma na kuongeza ubunifu ikiwa ni pamoja na kuboresha mitandao ya wizara katika masuala ya tovuti, blog na mitandao mingine ya kijamii na kwa upande wangu sikuwa na shaka na Temba katika masuala ya mitandao kwa kuwa alikuwa mtaalam katika eneo hilo na mafunzo yake ya muda mfupi aliyoyapata Delhi nchini India yalimuongezea ujuzi wa ziada.

Temba tulizidi kushauriana kwa kila changamoto aliyokuwa akiipata katika ofisi yake na katika jambo lililokuwa likimtatiza katika utendaji kazi ni kutoshirikishwa katika masuala yanayohusu habari na picha hasa katika matukio kwani ni eneo aliloona ndiyo linalomfanya aonekane kama anafanya kazi.  Akiwa hana muda mrefu wizara ya Maliasili na Utalii, Temba alitamani kuambatana na Waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo Profesa Jumanne Maghembe katika ziara zake ili aripoti matukio lakini haikuwa rahisi kwa kuwa waliokuwa naye ofisini hawakuamini haraka uwezo wake. Aliniomba ushauri juu ya hilo nilichomuambia ni kwamba aanze na matukio yanayofanyika hapo ofisini kwani viongozi watakapoona kazi yake suala la kuambatana na waziri atalipata tu.

Temba alifanya hivyo na kuhakikisha matukio yote ya wizara yanayofanyika Dar es Salaam taarifa zake zinatoka katika vyombo vya habari na mimi si kusita kumpa moyo pale tukio alilolifanya likitoka katika gazeti. Temba alianza ziara kwa kufanya kazi kwa ukaribu na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo Injinia Ramo Makani na kuhakikisha matukio mengi ya naibu waziri huyo yanatoka kwenye vyombo vya habari na mitando ya kijamii.

Siku moja waziri Maghembe alifanya ziara katika moja ya hifadhi na aliagiza afisa habari Temba aende katika ziara hiyo, Temba alinipigia simu na kunieleza kuwa ameambiwa aende kufanya kazi. Nilimkumbusha niliomwambia na kumueleza hapo anachotakiwa ni kufanya kazi maana Profesa Maghembe ameanza kumkubali. Temba alifurahi sana hasa baada ya kuona ndoto yake ya kufanya kazi na waziri mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii inatimia.

Wakati Temba anaanza kufanya kazi kwa ukaribu na profesa Maghembe ghafla kukafanyika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ambapo wizara ilipata waziri mpya Dk Hamis Andrea Kigwangwala na naibu Japhet Hasunga. Mabadiliko hayo yalimstua Temba kwa hofu kuwa alishaanza kuwa karibu Mawaziri hao wawili hivyo mabadiliko hayo yangefanya ichukue muda kuanza kujijenga kwa viongozi wapya.  Kama ilivyo kawaida yake Temba alinieleza mabadiliko hayo na kuniulizia juu ya Mawaziri hao wapya, mimi nilimueleza kuwa Kigwangala  simfahamu sana ingawa naelewa kuwa ni mchapakazi na mtumiaji mzuri wa mitandao ya kijamii  hivyo suala la matukio yake kutoka katika vyombo vya habari atalipa kipaumbele na wewe fursa hiyo utaipata. Kuhusu Naibu Waziri nilimueleza kuwa huyo simfahamu ila taarifa zake nazijua kupitia rafiki yangu kuwa ni mtu mzuri mwenye mawazo ya mbali hivyo nikamshauri aende kujitambulisha kwake atapata ushirikiano.

Haikupita wiki moja Temba alinipigia simu na kunieleza kuwa alitoka ofisi ya Naibu Waziri Hasunga na kujitambulisha ambapo walizungumza sana kwa takriban dakika arobaini na kubainisha kuwa mhe Naibu Waziri alionesha yuko ‘positive’ sana katika masuala ya matukio hivyo alidhani atafanya kazi naye vizuri. Siku moja Temba alinipigia simu na kunieleza kuwa watakuwa na ziara na mhe Hasunga. Kikubwa nilichomshauri ni kutumia nafasi hiyo kuonesha uwezo wake ili akubalike na viongozi hao. Temba alihakikisha katika ziara hiyo matukio ya Hasunga yanatoka katika vyombo vya habari na mimi katika kumsaidia nilihakikisha matukio yake yanayotoka katika magazeti nayapiga picha na kumtumia kwa njia ya whatsup na yeye kumpelekea mhe Naibu Waziri kwa njia hiyo. Kipindi kufupi Naibu Waziri Hasunga kazi zake zilianza kuonekana  naTemba kuanza kuwa maarufu  katika tasnia ya mawasiliano.

Naweza kusema ziara za Hasunga zimemfanya Waziri wa Maliasili na Utalii Kigwangala aone haja yeye kuambatana na Temba katika ziara zake. Uamuzi wa Kigwangala kuambatana na Temba ulimfurahisha sana na Temba hakusita kunieleza kuwa sasa mhe Waziri ameanza kunikubali hivyo itabidi nipige kazi. Kukubalika kwa Temba na Mhe Kigwangala kumefanya wawili hao kuwa karibu sana kiasi cha mimi kuona kuwa pamoja na kuwa sote tumeumia kwa kuondokewa na mpendwa wetu lakini mhe waziri ataumia sana kwa kuondokewa na mtu aliyemsaidia sana katika kazi zake hasa katika kuripoti matukio ya nyanja ya uhifadhi wa utalii wetu na itachukua muda kuwa na mtu wa aina hiyo.

Wakati wa uhai wake mara kadhaa tukiwa na Anthony Ishengoma Afisa Habari Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dar es Salaam na Dodoma tulizungumza sana na Temba kuhusiana na mahitaji ya viongozi hasa katika masuala ya kuripoti ziara zao na kuona haja ya kujifunza masuala mbalimbali yatakayofanya taasisi ione umuhimu wa uwepo wa Afisa Mawasiliano jambo lililomfanya kuwa karibu sana na sisi ili kujifunza.

Napenda kukiri wengi niliowasiliana nao mara baada ya kusambaa kwa taarifa ya kifo cha Temba akina Abdulwakil Saiboko Afisa Habari Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Hassan Mabuye Afisa Habari Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Fatna Mfalingundi Afisa Uhusiano Chuo Kikuu Mzumbe, Kondo Ally Afisa Habari Wizara ya Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Jamal Hashim mwandishi Kituo cha Runinga cha Azam wote tulishikwa na bumbuwazi ikiwa ni ishara ya kuonesha kuondokewa na mtu muhimu sana ambaye tulisoma Chuo kimoja lakini darasa na mwaka tofauti ingawa wengi wanaweza kudhani tulisoma pamoja kutokana na ukaribu wetu.

Temba ni kijana asiyepitia chumba cha habari lakini alipenda kujifunza sana na mchapakazi asiyependa kushindwa. Alikuwa mtu wangu wa karibu sana, tumekuwa tukipeana ushauri katika masuala mbalimbali yanayohusu tasnia ya mawasiliano. Nakumbuka kabla ya safari yake iliyochukua uhai wa maisha yake alinipigia simu akiwa Dodoma na tulizungumza kuhusu ajali iliyompata afisa habari mwandamizi wa viwanda na biashara shadrack Sagati.  Alinieleza uwepo safari ya Arusha na baadaye Mwanza huku nikimkumbushia jinsi alivyoweza kuripoti ziara ya pori kwa pori akiwa na mhe. Kigwangawala. Nilimueleza kuwa kazi na ‘coverage’ yake ilikuwa nzuri sana hivyo aendelee kuchapa kazi atafika mbali. Mazungumzo yetu yaliishia kwa kuniuliza lini nahamia Dodoma ili anifanyia mpango wa nyumba katika eneo analoishi area C, nilimueleza hatuna muda mrefu ila nitamfahamisha mambo yatakapokaa sawa, jibu lake aliniambia ‘’pamoja kaka’’. Huyo ndiyo Hamza Faidi Temba Afisa Habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

About regina

Check Also

3

HALMASHAURI YA WILAYA YA KISARAWE YAPITISHA BAJETI YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 30

Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Hamisi Dikupatile akizungumza na wajumbe wa kikao cha …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

eleven − one =