Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei
MKAZI wa Kijiji cha Kasisi wilayani Chunya mkoa wa Mbeya, Masanila Lukelesha (45) anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kusababisha kifo cha ndugu yake, Lutonja Lukelesha (33).
Akizungumzia kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema mtuhumiwa huyo anadaiwa kumsababishia majeraha yaliyopelekea Lutonja kufariki dunia, kwa kumpiga na fimbo akimtuhumu kuiba redio yenye thamani ya Sh. 15,000.
Kamanda Matei ameeleza kuwa, marehemu Lutonja alifariki dunia tarehe 22 Septemba 2018 akiwa anajipatia matibabu ya kienyeji nyumbani kwake.
“Inadaiwa kuwa marehemu alipigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kukanyagwa kwa miguu kifuani na tumboni siku ya tarehe 12.09.2018 majira ya saa 12:09 mchana huko kijiji cha Kasisi na kaka yake aitwaye Masanila Lukelesha [45] Mkazi wa Kasisi akiwa na wenzake wawili,” amesema na kuongeza Kamnda Matei.
“Chanzo cha tukio hili ni tuhuma za wizi wa radio ndogo yenye thamani ya Tshs 15,000/= ya mmalila mchoma mkaa ambaye jina lake halisi bado kufahamika. Msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa wengine wawili waliokimbia unaendelea.”