Tuesday , January 22 2019

Home / MCHANGANYIKO / Serikali Yatoa Rai kwa Wananchi Kuendelea Kuasili Watoto

Serikali Yatoa Rai kwa Wananchi Kuendelea Kuasili Watoto

PMO_7721

Waziri wa Utalii na Maliasili, Dkt. Hamisi Kigwangalla, akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini mheshimiwa Emmanuel Mwakasaka, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mheshimiwa Ummy Mwalimu leo bungeni. Waziri Kigwangala amejibu maswali ya wabunge kwa mara ya kwanza baada ya kutokuwepo bungeni kwa muda wa miezi mtatu kutokana na kupata ajali eneo la Magugu mkoani Arusha mwezi Agosti mwaka huu.

…………………..

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Serikali imetoa rai kwa wananchi kuendelea kuasili watoto ili kuwasaidia kupata huduma za msingi na malezi bora.

Rai hiyo imetolewa leo Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akijibu swali la Mhe. Fatma Toufiq lililohoji juu ya uhamasishaji wa jamii kuhusu kuasili watoto

Waziri Dkt. Kigwangalla amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuasili watoto kupitia vyombo mbalimbali vya habari na kupitia Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Mtoto pamoja na Program ya Ulinzi na Usalama.

“Juhudi hizo za Serikali zimewezesha jumla ya watoto 66 wakiwemo wa kiume 37 na wa kike 29 kuweza kuasiliwa hivyo tunatoa rai kwa wananchi kuendelea kuwasaidia watoto wengine kwa njia ya kuwaasili,” alisisitiza Mhe. Kigwangalla.

Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani wanaunganishwa na familia zao ili wapate huduma zote za msingi ikiwemo haki ya kulelewa na kutunzwa katika familia hivyo Serikali inashauri wananchi wenye nia ya kuasili watoto kuwasiliana na Maofisa Ustawi wa Jamii walio karibu ili kupewa utaratibu wa uasili.

Mhe. Kigwangalla amefafanua kuwa kwa mujibu wa taarifa ya utafiti ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani ya mwaka 2018 inaeleza kuwa jumla ya watoto 6,393 walitambuliwa katika Mikoa sita ambayo ni Dar es Salaam, Mbeya, Iringa, Dodoma, Arusha na Mwanza.

Aidha hadi kufikia Juni, 2018 jumla ya watoto 1,745 kati ya waliotambuliwa wamepatiwa huduma mbalimbali zikiwemo za kuunganishwa na familia zao, kurudishwa shuleni, kupatiwa stadi za maisha kuanzisha shughuli za ujasiriamali na kuwatafutia malezi mbadala ya kifamilia.

Waziri Kigwangalla amesema kuwa matunzo, malezi na ulinzi wa mtoto ni haki ya mtoto  na ni wajibu wa mzazi au mlezi kutekeleza jukumu la kumtunza mtoto kwa mujibu wa sheria.

 

About Alex

Check Also

_MG_9933

CCM PANGANI YAMTUNUKU TUZO YA SHUKRANI RAIS DKT MAGUFULI KWA UAMUZI WAKE WA KURIDHIA KUTIA SAINI UJENZI WA BARABARA YA TANGA-,PANGANI HADI BAGAMOYO

Mwenyekiti Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Pangani Hamis Mnegero akizungumza na waandishi wa habari …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

20 + 16 =