Tuesday , March 26 2019

Home / MCHANGANYIKO / VIDEO;Waziri Kakunda Atoa Maagizo Mazito Mtwara

VIDEO;Waziri Kakunda Atoa Maagizo Mazito Mtwara

1

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Joseph Kakunda, akisisitiza jambo kwa wawakilishi wa vikundi vya wabanguaji wadogo wa korosho (hawapo pichani). Kwenye kikao hicho Waziri Kakunda ameziagiza taasisi mbalimbali za serikali kuhakikisha zinafanya kazi pamoja kuwawezesha wabanguaji wadogo kushiriki zoezi la kubangua korosho zilizonunuliwa na serikali.

2

Mwakilishi wa Mandawa AMCOS kutoka Wilaya ya Ruangwa, Selemani Mwigambe, akiwasilisha hoja wakati wa kikao cha Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji na wawakilishi wa vikundi vidogo vya ubanguaji wa korosho kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi. Kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kilikuwa na lengo la kutambua changamoto za vikundi hivyo ili kuviwezesha kushiriki zoezi la kubangua korosho iliyonunuliwa na serikali.

3

  1. Baadhi ya wawakilishi wa vikundi vya wabanguaji wadogo wa korosho kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi wakifuatilia kwa makini maelekezo ya serikali yaliyotolewa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Joseph Kakunda(hayupo pichani) kwenye kikao chake na wawakilishi hao leo mjini Mtwara.

………………..

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Joseph Kakunda ameziagiza taasisi mbalimbali za serikali zihakikishe zinashirikiana kwa pamoja ili kutimiza azma ya serikali kuona wabanguaji wadogowadogo wa korosho wanashiriki kwenye zoezi la kubangua korosho iliyonunuliwa na serikali.

Kwenye kikao chake na wawakilishi wa vikundi mbalimbali vya kubangua korosho kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara, Waziri Kakunda amewaagiza Makatibu Wakuu wa wizara yake na ile ya Kilimo kwa kushirikiana na Makatibu Tawala wa mikoa hiyo miwili, wanahakikisha wabanguaji wadogo wanapewa ushirikiano kwa kupatiwa korosho za kubangua kutoka kwenye maeneo yao.

Kuhakikisha ubora wa korosho itakayobanguliwa na vikundi vya wabanguaji wadogo inakidhi viwango vya soko, mheshimiwa Kakunda amelitaka Shirika la Mendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele kwa pamoja wafanye ziara za kutembelea vikundi hivyo ili kujua changamoto zinazowakabili. “Jipangeni kuwatembelea kwenye maeneo yao mjiridhishe na kuona teknolojia wanazotumia  muwasaidie inapobidi ili ubora wa korosho itakayobanguliwa ulindwe na uwe mzuri” amesisitiza Waziri Kakunda.

Waziri Kakunda pia ameitaka SIDO ihakikishe inavisaidia vikundi hivyo vya ubanguaji mikopo ya mashine itakapothibitika kikundi kina uwezo kufanya kazi lakini hakina vitendea kazi.

Kuhusu kilio cha wakulima kudhulimiwa korosho wakati wa kupima, Waziri Kakunda ameagiza Wakala wa Vipimo (WMA) ianze mara moja zoezi la kuhakiki mizani zinazotumiwa kwenye maeneo ya kukusanya na kupima korosho. Waziri Kakunda amesema, “Wakala wa vipimo nchini watembelee maeneo yote yanayofanya ukusanyaji na upimaji wa korosho kwenye mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma na Pwani wajiridhishe kama vipimo vinavyotumika vinakidhi matakwa ya kisheria”.

Aidha amewataka Makatibu Tawala wa mikoa wahakikishe wanasimamia utekelezaji wa Sheria ya Ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999 ambayo inazitaka serikali za mitaa ngazi ya halmashauri kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi kila kijiji. Sheria hizo mbili zimetenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kijamii, kidini na kiuchumi. Utekelezaji wa sheria hizo utawanufaisha wabanguaji wadogo kwa kutenga maeneo watakayo kuwa wanafanya kazi zao bila bughudha.

Kwa upande wao wabanguaji wadogo wamepongeza hatua iliyochokuliwa na serikali ya kununua na kuhakikisha korosho zote zinabanguliwa nchini. “Uamuzi wa kushirikisha wabanguaji wadogo ni jambo la kupongezwa sana, hakika Rais Magufuli ni kiongozi wa wanyonge” amesema Bi. Daria Erasto, Mtendaji Mkuu wa Umoja wa Wabanguaji Wadogo wa Korosho Tanzania (UWWKT).

About Alex

Check Also

AA

RAIS MAGUFULI ATENGUA UTEUZI WA MKURUGENZI MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA (TAA)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

nineteen − 6 =