Saturday , March 23 2019

Home / BIASHARA / GAVANA BoT: ELIMU YA MASUALA YA FEDHA NI MUHIMU KATIKA MFUMO WA TAARIFA ZA MIKOPO

GAVANA BoT: ELIMU YA MASUALA YA FEDHA NI MUHIMU KATIKA MFUMO WA TAARIFA ZA MIKOPO

1

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Profesa Florens Luoga akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya  Kuelimisha umma kuhusu taarifa za mikopo na masuala ya fedha ambayo ni muhimu katika mfumo mzima wa taarifa za  mikopo uliofanyika jijini Dar es salaam leo.

2

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB na Mwenyekiti wa Mabenki Bw. Abdulmajid Nsekela akisaini kwenye bango wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya  Kuelimisha umma kuhusu taarifa za mikopo na masuala ya fedha.

3

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB  na Mwenyekiti wa mabenki Bw. Abdulmajid Nsekela pamoja na washiriki wengine wakiwa katika uzinduzi huo.

4

Wadau mbalimbali wakiwa katika uzinduzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa BoT jijini Dar es Salaam.

6

Meneja Msaidizi-Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki wa BoT, Bi. Vicky Msina na  Bi. Zalia Mbeo Meneja Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki (BOT) kushoto pamoja na waalikwa wengine wakiwa katika uzinduzi huo.

7

Baadhi ya wadau wakiwa katika uzinduzi huo uliofanyika leo kwenye ukumbi wa BoT jijini Dar es salaam.

…………………………………………………………………………..

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Profesa Florens Luoga  akimuwakilisha  mgeni rasmi  Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango kwenye uzinduzi  wa Kampeni ya  Kuelimisha umma kuhusu taarifa za mikopo amesema elimu kuhusu masuala ya fedha ni muhimu katika mfumo mzima wa taarifa za  mikopo.

Akiongea  katika uzinduzi wa kampeni hiyo leo kwenye ukumbi wa BoT jijini Dar es salaam amesema kampeni hiyo ya elimu kwa umma inalenga kuwaelimisha watumiaji wa  huduma za fedha na wadau wengine kukuza uelewa wao kuhusu taarifa za mikopo ili  kuongeza ushiriki katika matumizi ya taarifa za mikopo hapa nchini.

Kupeana taarifa za mikopo kunapunguza tofauti ya upatikanaji wa taarifa miongoni  mwa wakopeshaji na wakopaji na kupunguza gharama za kutafuta taarifa hizo na  kuboresha upatikanaji wa mikopo kwa sehemu kubwa ya wananchi.

Akifafanua zaidi wakati wa uzinduzi huo , Profesa Luoga amesema kampeni hiyo  ya uhamasishaji na elimu kwa umma kuhusu taarifa za wakopaji   imeandaliwa na BoT kwa kushirikiana na International Finance Corporation, ambao  ni mwanachama wa Kundi la Benki ya Dunia.

Ameongeza kuwa kampeni hiyo inaangalia masuala muhimu kuhusu taarifa za mikopo  ambazo ni pamoja na maana ya taarifa ya mikopo, kwa nini taarifa hizo ni muhimu  kwa wakopaji na wakopeshaji, namna gani watumiaji wa huduma za fedha wanaweza  kupata taarifa za mikopo, umuhimu wa kuwa na historia nzuri ya ukopaji na  umuhimu wa kuangalia taarifa zako za mikopo mara kwa mara kutoka taasisi  zinazoandaa taarifa hizo ili kuhakikisha taarifa za mikopo zinakuwa nzuri.

“Mpango huu ni sehemu ya mpango mpana zaidi wa kukuza elimu kuhusu masuala  ya fedha kwa lengo la kukuza huduma jumuishi za kifedha Tanzania kutoka asilimia  65 mwaka 2018 hadi asilimia 75 ya watu wazima wanaotumia huduma za kifedha  ifikapo mwaka 2022,”amesema.

Prof. Luoga amesema BoT ilizindua mfumo wa taarifa za mikopo Septemba mwaka  2012 ilipotoa kanuni zilizotokana na Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka  2006, yaani kanuni za Kanzidata ya Taarifa za Mikopo za mwaka, 2012 na Kanuni za Kampuni za Taarifa za Mikopo, 2012.

“Hivi sasa kuna taasisi mbili zinazoandaa taarifa za mikopo ambazo zimesajiliwa na  zinazofanya kazi hapa Tanzania. Taasisi hizo ni Dun & Bradstreet Credit Bureau  Tanzania Limited na Creditinfo Tanzania Limited,”amesema.

Amesema taasisi hizo zinapata taarifa zake kutoka Kanzidata ambayo inasimamiwa  na Benki Kuu ya Tanzania na taarifa (data) nyingine kutoka taasisi zingine zinazotoa  huduma mbalimbali, kama kampuni za simu, wakala wa kukusanya madeni, wauzaji  wa jumla na reja reja wanaotoa bidhaa na huduma kwa mkopo, taasisi za umma  kama vile Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Mamlaka ya Vitambulisho  vya Taifa (Nida) na Masijala za Mahakama.

Amesema taasisi zinazoandaa taarifa za mikopo hutayarisha taarifa hizo na kuzitoa  kwa wakopeshaji na watumiaji wengine kwa ada fulani wanapozihitaji ili kuweza  kujua hali ya kifedha ya watu wanaotaka kupata mikopo kutoka kwao na kwamba  taarifa za mikopo ni muhimu pia kwa watumiaji wengine, ikiwemo BoT kama  msimamizi na mdhibiti wa sekta ya fedha, wakala za serikali na sekta nyingine katika  uchumi kama waajiri, watoa huduma za bima, wauzaji wa jumla na reja reja,  kampuni za karadha na mawakala wa mikopo ya nyumba.

Prof.Luoga amesema pia kubadirishana  taarifa sahihi kati ya taasisi za fedha na  wadau wote ni muhimu katika mchakato wa maamuzi, kupunguza gharama ya  mikopo na wakopaji wasiolipa madeni yao. Katika kipindi cha muda mrefu, mfumo  huu unatarajiwa kuchangia kupunguza gharama za mikopo, mikopo chechefu na  kukuza uthabiti wa sekta ya fedha.

“Aidha, kushirikishana taarifa za mikopo kunachangia katika kujenga nidhamu ya  ukopaji kwa kuepuka kukopa bila sababu na kuchukua mikopo mikubwa. Kwa  wakopeshaji, taarifa za mikopo zinarahisisha kuangalia vihatarishi na kufanya  maamuzi bora wakati wa kutoa mikopo kwa taasisi na wajasiriamali wadogo pamoja  na kufuatilia wakopaji kwa ufanisi zaidi,”amesema.

Amefafanua faida za kuwaruhusu wakopaji kupata taarifa zao za mikopo ni kujenga  uaminifu, uwazi na usahihi wa taarifa. Ili kuhakikisha kwamba matakwa ya kisheria  na usimamizi na kukuza kukubalika kwa mfumo wa taarifa za mikopo, Benki Kuu ya  Tanzania inasimamia uendeshaji wa Kanzidata ya Taarifa za Mikopo na Taasisi zinazoandaa taarifa za mikopo.

Amesea BoT  imekuwa ikifanya kazi ya kukuza mfumo wa taarifa za ukopaji ili  kuboresha usimamizi wa vihatarishi vya mikopo katika benki na taasisi  za fedha na  taasisi nyingine zinazotoa mikopo, lengo likiwa ni kuongeza upatikanaji wa mikopo  na kukuza huduma jumuishi za kifedha.

Prof.Luoga amesema katika kufanya hivyo, pamoja na mambo mengine walihitaji  kupata msaada wa kitaalamu kutoka Benki ya Dunia kupitia shirika lake tanzu la  International Finance Corporation katika maeneo manne ambayo ni kuimarisha  uwezo wa Benki Kuu ya Tanzania kudhibiti na kusimamia shughuli za taarifa za  mikopo;

Hivyo amesema uzinduzi huo unaonesha jitihada za BoT na wadau wengine katika  kukuza uelewa kuhusu mfumo wa taarifa za mikopo na  elimu ya fedha kama vitu  muhimu katika uendeshaji wa soko la mikopo, uthabiti wa sekta ya fedha na  maendeleo ya uchumi wa taifa kwa ujumla.

“Inatarajiwa kupitia kampeni hii ya uhamasishaji, wadau mbalimbali watajua faida  za kutumia mfumo wa taarifa za mikopo. Ujumbe utaelekezwa kwa wakopeshaji na  wakopaji kwa lengo la kuongeza ufahamu juu ya umuhimu wa taarifa za mikopo na  faida kwa makundi yote mawili,”amesema.

About bukuku

Check Also

maxresdefault

HOTELI YA KWANZA ARUSHA YATENGA MILIONI KUMI KWA AJILI YA YATIMA

UONGOZI wa hoteli ya kitalii ya New Safari Hoteli ya jijini Arusha umefanikiwa kujiwekea utaratibu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

3 × one =