Saturday , March 23 2019

Home / BIASHARA / TRA kuvifungia viwanda vya pombe kali endapo havitatumia stempu za kielektroniki

TRA kuvifungia viwanda vya pombe kali endapo havitatumia stempu za kielektroniki

TBL MWANZA 5

Na Rachel Mkundai, Mwanza
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewata wazalishaji wote wa vileo nchini kutumia mfumo wa stempu kodi za kielktroniki katika viwanda vyao na endapo hawatafanya hivyo hadi kufikia tarehe 28 Februari, 2019 watafungiwa uzalishaji katika viwanda hivyo.
Akizungumza mara baada ya kutembelea viwanda vinavyozalisha vileo aina ya bia na pombe kali jijini Mwanza kwa lengo la kukagua ufungwaji wa mfumo wa Stempu Kodi za Kielektroniki (ETS), Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere amewataka wamiliki wote wa viwanda vinavyozalisha vileo nchini kuhakikisha wamefunga mfumo huo kwenye mtandao wa uzalishaji wa bidhaa zao ili serikali iweze kupata kodi stahiki.
“Nitoe wito kwa wamiliki wote wa viwanda vya vileo wahakikishe wanafunga huu mfumo wa Electronic Tax Stamp (ETS) ili kuepuka mambo ya kukwepa kodi”, amesema Kamishna Kichere,
Akiwa jijini Mwanza, Kamishna Mkuu Bw. Kichere ametembelea viwanda vya Tanzania Breweries Limited, (TBL) Serengeti Brerweries Limited (SBL), Mwanza Quality Wine na Premidis Limited ambapo akiwa katika kiwanda cha Premidis aligundua kuwa kuna katoni za pombe kali aina ya Shimla Waragi 10,786 ambazo ndani ya katoni hizo zilikutwa chupa ambazo hazikubandikwa stempu za ushuru wa bidhaa kutoka TRA, hii ikiwa na maana kwamba bidhaa hizo hazikulipiwa ushuru wa bidhaa ambao ni shilingi 3,315 katika kila lita moja ya pombe kali.
“Utaratibu ni kwamba ukishatengeneza bidhaa, unabandika stika ya TRA, ndipo upeleke sokoni, ukichukua kwa wastani utakuta kwamba ushuru wa bidhaa ambao ungekwepwa hapa ni takribani shilling 38.6m”, amesema Kamishna Kichere.
Naye meneja wa TBL tawi la Mwanza Bw. Joseph Malibe ameusifu mfumo wa Stampu Kodi za Kielektroniki na kusema kuwa ni mfumo wenye uwazi na unapunguza malalamiko katika ukadiriaji wa kodi kwa sababu unaonesha bidhaa zote zilizozalishwa na kodi yake kujulikana kwa TRA na mzalishaji.
“Kwa kweli mfumo huu ni mzuri na nitoe tu wito kwa wazalishaji wa vileo nchini kuutumia kwani utaondoa malalamiko katika ukadiriaji wa kodi, tulipe kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu’, alisema Bw. Malibe.
Aidha, Mkurugenzi wa Mwanza Quality Wines Bw. Leopald Lema ameunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kukusanya kodi na hivyo amepongeza TRA kuja na mfumo wa Stampu Kodi za Kieletroniki ambao unarahisisha ukusanyaji kodi katika biashara ya vileo.
“Hii ni njia nzuri na rahisi kwa serikali kukusanya kodi kieletroniki, na sisi wenye viwanda tunaitikia wito wa kufunga mfumo huu ili kuunga mkono ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo ya nchi yetu”, alisemaBw. Lema.
Ukaguzi huu unafanyika ili kutekeleza agizo la Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa TRA kuhusu kutafuta vyanzo vya mapato alilolitoa wakati wa kikao chake cha tarehe 10 Desemba, 2018 alipokutana na watumishi wa TRA, Wakuu wa Mikoa na viongozi wengine wa serikali katika ukumbi wa mwalimu Julius Nyerere na baadaye Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa kutoa melekezo kwa TRA alipokuwa akiwasilisha hoja ya kuhairisha bunge la 11 mnamo tarehe 9 Februari, 2019.
“Sambamba na hilo, naielekeza TRA kusimamia uwekaji wa mifumo ya kukusanya kodi za vileo kwa kutumia Stempu za Kodi za Kielektroniki kwa viwanda vinavyozalisha vinywaji hivyo, aidha ifikapo tarehe 28 Februari 2019 kila kiwanda kinachozalisha vileo kiwe kimeshafunga mfumo huo”, alisema Mhe. Waziri Mkuu Bw. Majaliwa alipokuwa akitoa maelekezo hayo.

About bukuku

Check Also

maxresdefault

HOTELI YA KWANZA ARUSHA YATENGA MILIONI KUMI KWA AJILI YA YATIMA

UONGOZI wa hoteli ya kitalii ya New Safari Hoteli ya jijini Arusha umefanikiwa kujiwekea utaratibu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

11 + eight =