Saturday , March 23 2019

Home / MCHANGANYIKO / MAELEKEZO YA WAZIRI WA NCHI TAMISEMI JUU YA UENDESHAJI WA MABASI YA DART

MAELEKEZO YA WAZIRI WA NCHI TAMISEMI JUU YA UENDESHAJI WA MABASI YA DART

IMG_20160418_114236

Kumekuwa na kusuasua kwa huduma ya usafiri wa Mabasi ya Mwendo Kasi jijini Dar es Salaam. Hali hii hainifurahishi hata kidogo ikichukuliwa kwamba wananchi wengi wamekuwa wakitegemea usafiri huu.

Tatizo hili limekuwa likijitokeza mara kwa mara na kuleta usumbufu kwa wananchi. Hata hivyo sijaona njia stahiki na ya kuridhisha zilizochukuliwa na watoa huduma hii katika kupatia ufumbuzi changamoto hii. Tatizo hili limekuwa likijitokeza mara kwa mara katika kituo cha mabasi cha Kimara wakati wa asubuhi na kituo cha mabasi cha Kivukoni na Gerezani wakati wa jioni. Imeonekena pia kuna wakati mabasi yanaonekana yakisafiri yakiwa tupu au yakiwa yameegeshwa pembeni ya vituo huku abiria wakiwa wamejazana katika vituo vya mabasi bila kujua hatima yao ya usafiri. Kutokana na hali hii natoa maelekezo yafuatayo:

1) Namuelekeza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo

haraka Eng. Leornard Lwakatare ahakikishe kwamba angalau mabasi kumi (10) ya ‘Feeder Road (maarufu kama bombardier) yanayobeba abiria kutoka Mbezi kwenda Kimara Mwisho yahamishiwe katika barabara ya mwendo kasi (inayoanzia Kimara hadi Kivukoni au Gerezani) ambapo angalau mabasi matano (5) yatakuwa kwa ajili ya abiria wa Kivukoni na angalau mabasi matano (5) yaliyobaki yatakuwa kwa abiria wa Gerezani. Kwa kuwa mabasi haya milango yake hairuhusu kupakia katika vituo vya mabasi ya mwendo kasi ya kawaida, hivyo basi mabasi haya yatachukua abiria wa moja kwa moja kutoka Kimara hadi Kivukoni au Gerezani, na wakati yanarudi Kimara yatachukua abiria wanaoshukia Kimara pekee.

2) Naelekeza Wakala wa Mabasi yaendayo Kasi DART wawasiliane

na SUMATRA ili mabasi ya kawaida yaongezwe kwa eneo la Kimara mpaka Mbezi ili abiria watakaoshuka Kimara wakitokea katikati ya jiji kuelekea Mbezi na wale watakaotoka Mbezi kuja Kimara kuweza kupata usafiri wa haraka.

3) Namuelekeza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo

haraka Eng. Leornard Lwakatare ahakikishe kwamba UDART ambaye ndio Kampuni yenye dhamana ya kusafirisha abiria ihakikishe inafanya matengenezo ya mara kwa mara ya mabasi yake ili kuondoa usumbufu unaojitokeza wa upungufu wa mabasi kutokana na mabasi mengi kuwa mabovu.

4) Vyombo vingine vya usafiri viache kutumia barabara za mwendo

kasi kwani kumekuwa na ajali nyingi zinazojitokeza ambazo zinasababisha mabasi ya mwendo kasi kupelekwa gereji mara kwa mara kwa matengenezo.

5) Mtendaji Mkuu wa DART awasilishe kwa Katibu Mkuu Ofisi ya

Rais – TAMISEMI majina ya watendaji wake walio chini yake ambao anahisi hawamsaidii ipasavyo kiushauri na kiutendaji ndani ya siku saba (7) ili wafanyiwe marekebisho kwa maslahi mapana ya Taasisi ya DART.

6) Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Ofisi ya Rais – TAMISEMI

ashirikiane na wataalamu wa Serikali Mtandao (EGA), Wizara ya Fedha na Wakala wa Mabasi yaendayo Kasi katika kulipatia ufumbuzi suala la matumizi ya Kadi ili kuepusha upotevu wa mapato unaotokana na matumizi ya tiketi za karatasi ambazo zimebainika kupoteza mapato mengi.

Naomba niwatoe hofu wananchi wote kwamba Serikali imeunda Timu Maalum inayofanya mapitio ya namna bora ya kuboresha mradi huu ambapo si kipindi kirefu sana changamoto mbalimbali zitakuwa zimepata ufumbuzi kupitia Timu hiyo ya wataalamu kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Wananchi mtaendelea kujulishwa pale mambo yote muhimu yanayoshughulikiwa kwa lengo la kuwawezesha wananchi kushiriki vema katika kujenga uchumi kupitia huduma bora ya usafiri itakayoboreshwa.

About Alex

Check Also

WAKITAZAMA

Waziri Biteko Asema Wizara Iko Tayari kuwahudumia Watanzania kutokea Ihumwa

Muonekano wa Jengo la Wizara ya Madini linalojengwa katika Mji wa Serikali eneo la Ihumwa.  …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four × 4 =